Na mwandishi wetu
Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa ambaye siku tatu zilizopita alisimamishwa kupisha uchunguzi dhidi ya uongozi wake amesema pamoja na yote lakini anajivunia kuona ngumi sasa zinapigwa kote nchini bila ya malalamiko.
Palasa na viongozi wenzake wa TPBRC walisimamishwa na serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ingawa kiongozi huyo anaendelea anajivunia mafanikio na kupungua malalamiko tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Palasa amezungumza hayo leo Ijumaa alipokuwa akihojiwa na Green Sports juu ya tuhuma zinazomkabili ambapo alisema kwa sasa hana lolote la kuzungumza.
Badala yake alisema kwamba anasubiri kujibu hoja zinazomkabili mbele ya tume ya uchunguzi iliyoteuliwa juzi na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro.
“Bado sijahojiwa na kamati kwa hiyo siwezi kusema lolote, sababu hata nikisema sasa itakuwa haisaidii, nasubiri kwanza waniite nizungumze nao kisha nitakuwa na lolote la kusema kuhusiana na hilo,” alisema Palasa.
Palasa ambaye ni bondia wa zamani alisisitiza kuwa anafurahi kuona ngumi zinapigwa sehemu nyingi Tanzania bila malalamiko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Huko awali kulikuwa na shida ya malipo lakini sasa watu wanapewa malipo yao, wanapata stahiki zao ndiyo maana hizo kelele hazipo, kilichobaki sasa ni mtu kulalamika inapotokea ameguswa kwenye masuala mengine binafsi lakini nafurahi kuona ngumi kama ngumi zinakwenda vizuri na hakuna malalamiko,” alisema Palasa.
Juzi Waziri Ndumbaro aliusimamisha uongozi TPBRC kupisha uchunguzi dhidi yao juu ya tuhuma zinazowakabili ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, ukiukaji wa katiba ya kamisheni na mgongano wa maslahi.
