Na mwandishi wetu
Waziri wa Maji, Juma Aweso (pichani) ambaye ni shabiki wa timu ya Simba, leo Alhamisi ameipongeza timu ya Yanga kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo yake wakati akifungua wasilisho la hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake ya Mwaka wa Fedha 2024/25.
Aweso aliisifia Yanga kwa ushindani mkubwa inaouonesha kiasi cha kuwaacha mbali wapinzani wake kwa kudumu katika kwango cha juu kwa muda mrefu.
Waziri huyo pia aliitaka Simba iendelee kujipanga kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao akiamini wanachokutana nacho sasa ni mapito tu.
“Mheshimiwa Spika, naomba nitoe pongezi za dhati, kwa kuwa tupo kwenye dunia ya ushindani mtu anapofanya vizuri ni vyema kuwapongeza, nitumie nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kuipongeza Dar Young Africans (Yanga) kwa kuendelea kusambaza maji nchi nzima.
“Mnyoge mnyongeni haki yake mpeni, kwa Yanga hii haikamatiki wala haishikiki, niseme wazi kabisa wenzangu wa Msimbazi tuendelee kujipanga kwa kuwa sisi ni chama kubwa, tutajipanga vizuri na tuendelee kuvumilia, nina imani haya ni mapito tu,” alisema Aweso huku akishangiliwa na wabunge wengine bungeni hapo.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC wanaongoza ligi hiyo kwa pointi 68 baada ya mechi 26 huku ikiwa haijafungwa katika mechi nane mfululizo za ligi inayoshiriki ikiwemo ile ya Kombe la Shirikisho CRDB ambayo ipo hatua ya nusu fainali, ikisubiri kuumana na Ihefu.
