Los Angeles, Marekani
Mwenyekiti na mmiliki wa klabu ya Chelsea, Todd Boehly amemtetea kocha wa timu hiyo, Mauricio Pochettino (pichani) akisema kiwango bora cha hivi karibuni ni ushahidi kuwa timu hiyo inaelekea pazuri chini ya kocha huyo.
Chelsea haijapoteza mchezo hata mmoja katika mechi tatu zilizopita ikiwa imezifunga West Ham na Tottenham Hotspur baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Aston Villa.
Matokeo hayo yameisaidia Chelsea kupanda hadi nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu England (EPL) ikiwa imezidiwa pointi mbili na Newcastle inayoshika nafasi ya sita na ipo katika nafasi nzuri ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Boehly amekuwa akishutumiwa kwa maneno ya kejeli na baadhi ya mashabiki hasa mwezi Machi mwaka huu lakini tajiri huyo wa nchini Marekani amesema kwamba sasa mipango ya bodi inaanza kuzaa matunda.
“Tumeona katika mechi mbili tatu zilizopita, kipindi cha pili dhidi ya Aston Villa (sare ya 2-2) na dhidi ya Tottenham (ushindi wa 2-0) na dhidi ya West Ham (ushindi wa 5-0) tulicheza soka zuri,” alisema Boehly.
Boehly aliisifia timu yake katika mechi hizo kwa namna wachezaji walivyoonekana kucheza kwa mpango, mashuti waliyoyapeleka kwenye lango la timu pinzani vyote vikionesha jinsi timu inavyokuwa vizuri.
Tajiri hiyo aliongeza kwa kusema kuwa matokeo ya mechi hizo yamebadili hata hoja za wachambuzi kuhusu timu hiyo mambo ambayo hata yeye yanamfanya kuamini kuwa Pochettino anafanya kazi nzuri.
