Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC, Yanga wameendeleza vyema dhamira yao ya kulitetea taji la ligi hiyo baada ya kuilaza Kagera Sugar bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Jumatano hii kwenye dimba la Azam Complex, Dar es Salaam.
Bao pekee lililoing’arisha Yanga katika mchezo huo lilifungwa katika dakika ya 82 mfungaji akiwa ni Mudathir Yahya ambaye aliitumia vyema pasi ya Aziz Ki kubadili matokeo ya mchezo huo.
Kama kawaida yake, Mudathir baada ya kufunga bao hilo alishangilia kwa staili yake iliyozoeleka ya kama mtu anayezungumza na simu na hivyo kuwazidishia furaha mashabiki wa Yanga ambao baadhi yao walianza kuingiwa na hofu ya timu yao kushindwa kutoka uwanjani na pointi zote tatu.
Kwa ushindi huo, Yanga inakuwa imefikisha pointi 68 na imebakisha mechi mbili ambazo inatakiwa ipate ushindi ili kujihakikishia ubingwa wa ligi hiyo, ubingwa ambao pia unasakwa na Azam iliyo nafasi ya pili na Simba inayoshika nafasi ya tatu ambao kwa pamoja wanaomba Yanga wateleze katika mechi zilizobaki.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, KMC ilishindwa kutamba mbele ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma baada ya kunyukwa mabao 3-0.
Soka Yanga yaipiga Kagera 1-0
Yanga yaipiga Kagera 1-0
Read also