Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma amesema kupoteza kwao mechi dhidi ya Simba kwa mabao 2-0, kumetokana na uwepo wa faida ya timu kubwa ya Simba na si vinginevyo.
Akifafanua hilo Djuma alisema katika mabao waliyofunga Simba katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatatu hii kwenye dimba la Azam Complex, Dar es Salaam, hakukuwa na bao lolote lolote la kimbinu.
“Unapocheza na timu kubwa faida inakuwa kwao, kwanza wapo nyumbani, sisi tunataka matokeo na wao wanataka matokeo lakini faida wanaipa timu kubwa, tunaelewa huo ndiyo mpira acha tusahau hilo tuna mechi na Mtibwa (Sugar) na yaliyojiri tumeyasahau sababu unapocheza na timu kubwa haya yanatokea.
“Hatukufungwa kimbinu ilikua ni makosa yetu wenyewe, bao la kwanza ilipaswa kila mtu atembee na mtu sababu tunajua huwa Simba wana wachezaji wa kuruka vichwa lakini haikuwa hivyo.
“Goli la pili tumefunga sisi refa kaacha, wachezaji wamezembea wakitaka lile goli lililofungwa, wakapiga (Simba) ‘counter-attack’ wakafunga na hapo hakuna mbinu yoyote, lakini tunaelewa tumecheza na timu kubwa na ndiyo wakati wao huu na hatuna budi kuendelea na safari,” alisema Djuma.
Naye kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema: “Ninashukuru wachezaji wangu kwa namna walivyojitoa mpaka tumepata alama tatu muhimu na kubwa zaidi ni mchezaji wangu wa 12, mashabiki waliojitokeza kuja kutusapoti na tumemaliza salama na sasa tunajipanga na Azam.
“Mechi na Azam ni mechi ngumu kama inavyofahamika, tunashindana kwa kufuatana katika msimamo. Ni mechi yenye taswira itakayoonesha nani atakuwa wapi na tunaenda kujipanga dhidi yao kuhakikisha tunapata matokeo yaliyo mazuri.”