Na mwandishi wetu
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amesema kwa sasa kikubwa kinachowapa nguvu ya kupambana ni namna mashabiki wao wanavyohitaji ushindi katika kila mchezo na kufanya kila mechi iliyo mbele yao iwe kama fainali.
Mwamnyeto amezungumzia hayo baada ya timu hiyo jana Jumapili kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuendelea kujichimbia kileleni ikifikisha pointi 65 baada ya mechi 25, ikiiacha Azam katika nafasi ya pili kwa pointi 54 ilizovuna katika mechi 24 na Simba iliyopo nafasi ya tatu kwa pointi 50 baada ya mechi zake 23.
“Kikubwa kinachotupa nguvu ni mashabiki wetu, kila mechi wanataka ushindi na mpaka sasa tuko kwenye mwelekeo wa kuchukua ubingwa, kwa hiyo kwetu wachezaji tunafanya kila mchezo kuwa ni fainali, mfano tumekuja Kigoma kucheza na timu ngumu ya Mashujaa, ndio imepanda daraja lakini ina wachezaji wazoefu na wapambanaji lakini mwisho tumefanikiwa kushinda,” alisema Mwamnyeto.
Beki huyo alisema hata kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakizungumza kauli moja ya ushindi na pointi tatu na hiyo ndio azma yao kubwa na kisha wataangalia mwisho wa ligi kilichopatikana.
Yanga inatarajiwa kutua Dar es Salaam leo Jumatatu ikitokea Kigoma ambapo wachezaji watatawanyika nyumbani kwao kisha kesho Jumanne kuanza maandalizi ya mchezo wao wa keshokutwa dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
