Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp na mshambuliaji wake, Mohamed Salah inaonekana hawana uhusiano mzuri baada ya kuzozana jana Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya West Ham.
Katika mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2, Salah alionekana kama kutoleana maneno yasiyo mazuri na Klopp wakati akijiandaa kuingia uwanjani akitokea benchi katika dakika ya 79.
Klopp baadaye alisema kwamba hawezi kuweka wazi mzozo ulioibuka baina yake na mchezaji huyo ingawa kilicho wazi ni kwamba hali haikuwa shwari baina ya wawili hao.
Akizungumzia tukio hilo, mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Peter Crouch alisema kwamba halikuwa jambo zuri kwa timu hiyo.
“Salah ni mchezaji ambaye katika mechi nyingi za Liverpool amekuwa akianza tangu kipindi cha kwanza na atakuwa mwenye hasira kwa kuanzia benchi,” alisema Crouch na kuongeza kuwa hakuna mtu anayependa kuona jambo kama hilo kwa kocha na mchezaji wake muhimu.
Kilichoonekana kwa Salah ni kama vile alichukizwa na jambo aliloambiwa na Klopp wakati akijiandaa kuingia uwanjani na alitaka kuendeleza mzozo huo lakini wachezaji wenzake, Darwin Nunez na Joe Gomez waliingilia kati na kumlazimisha aondoke.

Salah baada ya mechi alisema kama angeamua kuzungumza ‘moto ungewaka’ wakati Klopp alisema kwamba suala hilo lilizungumzwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na limekwisha.
Sare hiyo ya mabao 2-2 iliyoipata Liverpool inazidi kuiweka timu hiyo pagumu kwenye mbio za kulisaka taji la EPL kwani inabaki katika nafasi yake ya tatu na inachoomba sasa ni Man City na Arsenal ziharibikiwe katika mechi zao.