Na mwandishi wetu
Simba Queens imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) baada ya kuwalaza mahasimu wao Yanga Princess kwa mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Alhamisi hii jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Queens walianza kuandika bao la kwanza dakika nne baada ya mapumziko mfungaji akiwa ni Aisha Mnuka.
Dakika 16 baada ya kuingia bao hilo, Princess walijikuta wakichapwa bao la pili lililofungwa na Jentrix Shikangwa, bao ambalo liliwafanya baadhi ya mashabiki kuamini kuwa mechi hiyo ingeisha kwa matokeo hayo.
Hali hata hivyo ikawa tofauti baada ya Aisha kwa mara nyingine kuipatia Queens bao la tatu katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza (90+2) kabla ya mpira kumalizika.
Princess nao hawakukata tamaa kwani katika dakika hizo hizo za nyongeza, dakika ya tano (90+5) walifanikiwa kupata bao pekee la kufutia machozi lililofungwa na Kaeda Wilson.
Ushindi huo unawafanya Queens kuendeleza ubabe dhidi ya Princess katika msimu huu kwani katika mechi ya mzunguko wa kwanza, timu hiyo pia ilitoka uwanjani na ushindi kama huo.
Queens pia wanaendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo wakiwa wamekusanya jumla ya pointi 34 katika mechi 12 wakati Princess wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 21 nyuma ya JKT Queens wanaoshika nafasi ya pili.
Soka Simba Queens yaitesa Yanga Princess
Simba Queens yaitesa Yanga Princess
Read also