Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema anafahamu mashabiki wa timu hiyo wanaumia kwa matokeo ya timu hiyo ya hivi karibuni lakini amewaomba radhi na kuwataka washikamane wakati huu ili kujinasua hapa walipo.
Matola amezungumza hayo leo Jumatano akiwa Zanzibar, baada ya timu hiyo kufanya vibaya hivi karibuni wakianza kwa kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali.
Simba pia katika hatua hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB wametolewa kabla ya wikiendi iliyopita kufungwa mabao 2-1 na mahasimu wao Yanga kwenye Ligi Kuu NBC.
“Ni kweli siku zote mashabiki huwa wanaumia hasa tunapopoteza sababu siku zote shabiki anapenda furaha, ila kikubwa ninachowaambia kwanza tuwaombe radhi kwa kuwaumiza lakini ndio safari ya mpira ilivyo, siku zote huwezi kwenda kwa njia moja. Kimsingi tuwe pamoja katika kipindi hiki kigumu ili tujinasue na kurejea katika sehemu salama,” alisema Matola.
Pia, kocha huyo ameeleza kuwa wamekubali kushiriki michuano mipya ya Kombe la Muungano inayoanza leo Jumatano kutokana na kuhitaji kujipanga upya baada ya kufungwa na Yanga.
Alisema anaamini hakuna aliyefurahishwa na hilo hivyo watatumia kama ni kipindi cha kukaa sawa na kuelekezana wanapokosea ili wafanye vizuri katika mechi zilizobaki.
Matola pia amesisitiza kuwa wako kwenye michuano hiyo kwa ajili ya kupambana na kuhakikisha wanabeba ubingwa wa michuano hiyo ambayo kwa msimu huu inashirikisha timu nne pekee na mechi zikianzia hatua ya nusu fainali.
