Manchester, England
Kocha wa zamani wa Man United, Jose Mourinho amesema angeweza kuwa na matokeo mazuri kama angeaminiwa na kupewa ushirikiano kama ilivyo kwa kocha wa sasa wa timu hiyo, Eric ten Hag.
Mourinho aliwahi kuwa kocha Man United kati ya mwaka 2016 hadi 2018 na kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji ya Europa na Carabao lakini alitimuliwa Desemba 2018 wakati timu hiyo ikionekana kuhaha kusaka tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza na chanzo kimoja cha habari, Mourinho alisema maelewano yake na aliyekuwa mtendaji mkuu wa klabu wakati huo, Ed Woodward yalifanya kuwe na ugumu kupata matokeo mazuri.
“Uhusiano wangu na Ed Woodward ulikuwa mzuri, ni mzuri katika mambo binafsi, hata sasa huwa tunawasiliana kwa ujumbe mfupi lakini katika kazi haukuwa mzuri,” alisema.
“Mimi ndivyo nilivyo, ni mtu wa soka, Ed anatoka katika taaluma nyingine na anachokipata Ten Hag kwa sasa mimi sikuwa nikikipata,” alisema Mourinho.
Mourinho, kocha wa zamani wa Chelsea, Real Madrid, Tottenham, Inter Milan na AS Roma alifafanua kuwa hakuwa akipata ushirikiano na kuaminiwa kwa kiwango kizuri hali iliyomfanya ajione mnyonge kwani ilikuwa kama yuko katika hatua za mwanzo za kuyafanyia kazi baadhi ya mambo.
“Nadhani kama wangeniamini na kunipa ushirikiano kwa uzoefu wangu mambo yangeweza kuwa tofauti,” alisema Mourinho.
Mourinho pia aliongeza kwa kusema kuwa kuna baadhi ya wachezaji katika kikosi cha Man United ambao alitaka kuachana nao wakati akiwa kocha kutokana na tatizo la kutokuwa profesheno na kusisitiza kwamba katika hilo muda wakati wote husema ukweli.
