Na mwandishi wetu
Kombe la Muungano limerejea tena nchini ikiwa imepita miaka 20 tangu kusimama kwa mashindano hayo yanayotumia siku chache yakizishirikisha timu za Zanzibar na Tanzania Bara.
Kurejea kwa michuano hiyo kumeelezwa rasmi kupitia taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Zanzibar (ZFF) wakieleza mashindano hayo yataanza Aprili 24.
Mashindano hayo ambayo yatahitimishwa Aprili 27, mwaka huu, yatafanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikiwa ni kuelekea kilele cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Michuano hiyo kwa msimu huu itashirikisha timu nne zilizothibitisha kushiriki ambapo mbili za Bara; Simba na Azam FC wakati Zanzibar itawakilishwa na mabingwa wa kisiwani humo, KMKM na KVZ.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC Yanga, imeelezwa kuwa waliomba kutojumuishwa kwenye mashindano hayo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kubanwa na ratiba.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, KVZ itafungua dimba Aprili 24 dhidi ya Simba katika nusu fainali ya kwanza wakati nusu fainali ya pili itachezwa Aprili 25 baina ya Azam na KMKM na fainali itapigwa Aprili 27, mwaka huu ambapo mechi zote tatu zitaanza majira ya saa 2.15 usiku.
Soka Kombe la Muungano larudi
Kombe la Muungano larudi
Related posts
Read also