Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kuinyanyasa Simba katika Ligi Kuu NBC baada ya leo Jumamosi kuichapa mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga ambao wana rekodi ya kuichapa Simba mabao 5-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza, leo ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa kwa penalti na Stephanie Aziz Ki dakika ya 20 na kumfanya afikishe mabao 15 katika ligi hiyo.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Ahmed Arajiga baada ya beki wa Simba, Hussein Kazi aliyeingia kuchukua nafasi ya Henock Inonga aliyeumia, kumchezea rafu Aziz Ki ambaye alikuwa akieleleka kuonana na mlinda mlango wa Simba, Ayoub Lakred.
Simba walipachikwa bao la pili dakika ya 37 lililofungwa na Joseph Guede ambaye aliiwahi pasi ndefu ya juu iliyopigwa na Khalid Aucho kabla ya kuutuliza mpira na kumsogelea kipa Lakred ambaye juhudi zake za kumzuia Guede hazikuzaa matunda.
Simba waliendelea kupambana lakini juhudi zao zilishindwa kuwapa matokeo tofauti na hadi timu zinakwenda mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.
Bao pekee la Simba lilipatikana dakika ya 73 mfungaji akiwa ni Freddy Koublan ambaye aliinasa pasi ya Clatous Chama na kutuliza mpira kabla ya kuukota kidogo na kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga na hatimaye kuujaza wavuni kwa shuti kali.
Mchezo wa leo licha ya Simba kupoteza lakini kila timu ilionesha ushindani ambapo katika dakika ya 30, Saido Ntibazonkiza alimuunganishia pasi Kibu Dennis ambaye juhudi zake hazikufua dafu mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga.
Yanga nao walijibu mapigo dakika mbili baadaye lakini Clement Mzize alishindwa kuitumia vyema pasi ya Aziz Ki kuipatia timu yake bao.
Simba walionekana kuamka katika dakika za mwisho wakisaka bao la kusawazisha hali ambayo iliwafanya wachezaji wa Yanga kuwa na kazi ya ziada kudhibiti mashambulizi hayo.
Yanga pia walianza kumlalamikia mwamuzi Arajiga kwa imani kwamba muda wa dakika tano za nyongeza alioutoa ulikuwa umekwisha.
Kwa matokeo hayo Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 58 katika mechi 22 na kujiweka katika mazingira mazuri ya kulitetea taji hilo kwa mara ya nne mfululizo wakati Simba inabaki na pointi zake 46 katika mechi 21..
Soka Yanga yainyanyasa tena Simba
Yanga yainyanyasa tena Simba
Read also
