Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji mkongwe wa Brazil, Romario ambaye kwa sasa ana miaka 58, amejisajili kuichezea timu ya daraja la pili ya America FC ya Rio de Janeiro, klabu ambayo yeye pia ni rais wake.
Romario ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Brazil kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani, usajili wake ulipitishwa juzi Jumanne na sasa yuko tayari kuichezea timu hiyo.
Ligi hiyo ya Rio de Janeiro inaanza kutimua vumbi Mei 18 ambapo, Romario anasubiriwa kuweka rekodi ya kucheza soka la ushindani akiwa na umri mkubwa katika ligi hiyo huku ikielezwa kwamba mkongwe huyo atakuwa akilipwa mshahara wa kawaida.
Mamlaka inayosimamia soka Rio de Janeiro ilithibitisha usajili kukamilika kwa usajili wa Romario katika timu ya America FC na kwamba mshahara wa mchezaji huyo utachangiwa na klabu hiyo.
Romario hata hivyo hakuweka wazi ni lini hasa ataichezea klabu hiyo ingawa alisema si nia yake kucheza mechi za ligi hapo hapo akasisitiza kwamba angependa acheze pamoja na mwanaye, Romarinho ambaye ni mshambuliaji.
Mara ya mwisho, Romario kuonekana uwanjani kwenye mechi rasmi ilikuwa Novemba 2009 alipoichezea klabu ya America FC, klabu ambayo pia ni kipenzi cha baba yake, Edevair.
Tangu mwaka 2009, Romario amekuwa rais wa America FC na miaka mitano baadaye alichaguliwa kuwa seneta wa Rio de Janeiro.
Romario aliibukia katika timu ya soka ya vijana ya Vasco da Gama kabla ya kutimkia Ulaya ambapo alizichezea kwa mafanikio klabu za PSV Eindhoven na Barcelona na nyinginezo.
Mwaka 1994 alishinda tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa, tuzo ambayo aliipata kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kwa timu ya taifa ya Brazil hadi kubeba Kombe la Dunia.
Kimataifa Romario arudi uwanjani akiwa na miaka 58
Romario arudi uwanjani akiwa na miaka 58
Related posts
Read also
