Na mwandishi wetu
Baada ya matokeo ya 0-0 jana Jumatano dhidi ya Mashujaa, kocha msaidizi wa Azam, Yuoussuf Dabo amesema walipambana na kufanya kila kitu ili kushinda mchezo huo lakini wapinzani wao walisimama imara na mwisho wamekubali kuvuna pointi moja.
Azam ilipata matokeo hayo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kupunguza utofauti wa pointi moja pekee na kinara Yanga mwenye pointi 56 baada ya mechi 21 dhidi yao wenye pointi 51 kwa mechi 23.
“Haiwezekani kushinda kila mchezo, tumejaribu kushinda, timejaribu kucheza vizuri lakini wapinzani nao walikuwa vizuri. Ni kweli inawezekana kushinda kila mchezo lakini lazima ukubali kuwa kuna muda unakutana na mpinzani ana wachezaji wazuri pia.
“Kwa hiyo tunakubali na tunaendelea kupambana na mechi zijazo ingawa matokeo haya yametufunza kitu na tunapaswa kubadili mawazo yetu kuhusu ushindi na kuendelea kupambana bado safari haijaisha,” alisema Dabo.
Naye kocha mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ ambaye timu yake imepanda kwa nafasi moja ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 22, alisema kucheza kwa mitego na dhamira yao ya kutopoteza mechi hiyo, viliwasaidia kuondoka na pointi moja ugenini.
“Tuliingia uwanjani kwanza hatukutaka kupoteza mechi kwa kufahamu Azam ni timu nzuri ina matokeo mazuri, kwa hiyo tunaamini tukifanya makosa watatuadhibu kwa makosa yetu,” alisema Baresi.
Baresi apia alisema kwamba hata timu yake ilitengeneza nafasi muhimu na kukosa alama tatu zilizokuwa muhimu zaidi ila wanashukuru wamepata pointi moja kwa kuwa mechi hiyo ilikuwa na ufundi zaidi.
