Barcelona, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernández amemlalamikia mwamuzi kwa kumpa kadi nyekundu mchezaji wake, Ronald Araújo kuwa ndiyo sababu iliyochangia timu yake kufungwa mabao 4-1 na PSG na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ushindi wa PSG umekuja saa takriban 24 baada ya kocha wa timu hiyo, Luis Enrique kusema kwamba ana matumaini ya timu yake kuishinda Barca na kufuzu hatua ya nusu fainali ya ligi hiyo.
Xavi ambaye timu yake ilikuwa nyumbani alikiita majanga kitendo cha mwamuzi Istvan Kovacs kumpa kadi Araujo dakika ya 29 kwa kumchezea rafu, Bradley Barcola wakati Barca ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo, Barca inakuwa imetolewa katika ligi hiyo kwa jumla ya mabao 6-4 licha ya kupata ushindi wa mabao 3-2 katika mechi ya kwanza iliyopigwa mjini Paris na sasa PSG inasubiri kuumana na Borussia Dortmund katika nusu fainali.
Mabao ya ushindi ya PSG yalifungwa na Kylian Mbappe aliyefunga mawili pamoja na Ousmanne Dembele na Vitinha wakati bao pekee la Barca lilifungwa na Raphinha mapema dakika ya 10.
“Tumekerwa, kadi nyekundu ndiyo iliyoamua mchezo, tulikuwa tumejipanga vizuri, ilikuwa ni 11 kwa 11, kadi ilibadili kila kitu, kwangu mimi mwamuzi alikwenda mbali kwa kumpa kadi Araujo,” alisema Xavi.
“Kwa hakika mwamuzi alikuwa mbaya, nilimwambia, alikuwa janga, aliua mchezo, huwa sipendi kuzungumza kuhusu waamuzi lakini ilikuwa lazima kusema, sikuelewa,” alisema Xavi.
Xavi aliongeza kuwa halikuwa jambo zuri kubaki na wachezaji 10 kwa kuwa kuanzia hapo mchezo ukaanza kuwa tofauti na kwa vyovyote wanavyoweza kuuzungumzia mchezo huo, kadi nyekundu ndio kila kitu.
“Ni aibu, kazi ngumu iliyofanywa kwa msimu mzima inamalizika kwa sababu ya maamuzi ya mwamuzi mmoja, nilipenda mechi iwe ya wachezaji 11 kwa 11 mwanzo hadi mwisho, lakini imetolewa kadi nyekundu ambayo haikuwa na ulazima,” alisema Xavi.
Xavi naye baadaye kipindi cha pili alipewa kadi nyekundu wakati akipinga maamuzi ya kuinyima Barca penalti baada ya Marquinhos kumchezea rafu Ilkay Gundogan ingawa alikubali kujibebesha lawama kwa kadi hiyo akidai lilikuwa kosa lake.
Mechi za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zitapigwa kati ya Aprili 30 na Mei Mosi na marudiano itakuwa ni Mei 7 na 8 ambapo PSG itaumana na Borussia Dortmund wakati mshindi kati ya Man City na Real Madrid ataumana na mshindi wa mechi ya Arsenal na Bayern Munich.
Matokeo mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya
Barcelona 1-4 PSG
B Dortmund 4-2 Atl Madrid
Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano
Bayern Munich v Arsenal
Man City v Real Madrid
