London, England
Baada ya Arsenal kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Aston Villa, kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta amewataka wachezaji wake kusimama imara na kuhakikisha matokeo mabaya ya mechi moja hayawavurugii msimu wao.
Arsenal ikiwa nyumbani Emirates Jumapili hii ililala kwa mabao 2-0 mbele ya Villa katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) mabao ya washindi yakifungwa na Leon Bailey na Ollie Watkins.
Matokeo hayo mbele ya mtazamo wa baadhi ya mashabiki ni kama yametingisha matarajio ya Arsenal kubeba taji la EPL msimu huu na kuibua dalili za Man City kubeba taji hilo mara ya tano mfululizo kama watashinda mechi zao sita za mwisho.
Arsenal kwa sasa inakabiliwa na mechi mbili ngumu, Jumatano itaelekea mjini Munich kuumana na Bayern Munich katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza.
Baada ya hapo itakuwa na kibarua kingine kigumu cha EPL ugenini dhidi ya Wolverhampton Wanderers, timu ambayo mapema msimu huu ilijijengea heshima kwa kutoa vichapo mbele ya Man City na Tottenham.
Arteta pamoja na mazingira hayo amekataa kuitoa timu yake katika mbio za kulisaka taji la EPL msimu huu akiamini matokeo mabaya ya mechi moja hayatoshi kuwa sababu ya kuiyumbisha timu yake.
“Kama mechi moja inaweza kufanya hivyo hiyo maana yake ni kwamba sisi hatupo imara kiasi cha kutosha, ni hivyo tu, labda kwa mechi tatu, nne au zaidi,” alisema Arteta.
Arteta alisema kipindi cha kwanza timu yake ilicheza katika kiwango kizuri dhidi ya timu aliyoitaja kuwa ni bora lakini mambo yalibadilika kipindi cha pili.
Alisema katika kipindi hicho hawakuweza kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi kama kwenye kipindi cha kwanza na hatimaye timu yake kukubali kufungwa mabao mawili na kupoteza mchezo.
Matokeo ya mechi za ELP za Jumapili…
Liverpool 0-1 Crystal Palace
West Ham 0-2 Fulham
Arsenal 0-2 Aston Villa
