Na mwandishi wetu
Simba nayo imeungana na hasimu wake Yanga kwa kuaga fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Al Ahly ya Misri mjini Cairo.
Kwa matokeo ya mechi hiyo iliyopigwa usiku wa kuamkia Jumamosi hii, Simba inakuwa imetolewa kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba hata hivyo ilionesha upambanaji wa hali ya juu kwa kucheza pasi kadhaa na kulisakama mara kadhaa lango la Ahly na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalikuwa sare ya 0-0.
Mambo yaliwaharibikia Simba dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili walipofungwa bao la kwanza mfungaji akiwa Amr El Soleiya aliyefunga bao hilo kwa shuti kali akiwa ndani ya 18.
Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Maloul aliyemzidi ujanja Shomary Kapombe na kumuunganishia pasi Antony Modeste ambaye alimtengea vizuri El Soleiya naye bila ajizi akaujaza wavuni.
Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kupambana ingawa safu yake ya ulinzi ilionekana kushindwa kujipanga hasa upande wa kulia ambapo, Kapombe mara kadhaa alijikuta katika wakati mgumu kukabiliana na wachezaji wa Ahly walioonekana kutumia upande wake zaidi kwa kupeleka mashambulizi.
Dakika ya 64 nusura, Ahly waongeze bao la pili ambalo Modeste alikuwa akielekea kuonana na kipa Ayoub Lakred lakini Henock Inonga akawa makini kumdhibiti.
Dakika moja baada ya kosa kosa hiyo, Kibu Denis aliunganishiwa pasi na Mohamed Hussein na kukimbia kwa kasi na mpira lakini wakati akitaka kuwatoka mabeki wa Ahly alianguka na mwamuzi akampa kadi ya njano kwa kilichoonekana kama alijiuangusha na kuukumbatia mpira.
Wachezaji wa Simba waliendelea kuonesha utulivu wakizuia mashambulizi ya Ahly na kulisogelea lango la timu hiyo lakini mambo yaliwaharibikia kwa mara nyingine dakika moja kabla ya mpira kumalizika walipofungwa bao la pili.
Bao hilo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Mahmoud Kahraba, penalti ambayo ilitolewa baada ya Che Malone kumpiga kichwa Hussein El Shehata wakati wakiwania mpira wa juu.
Tukio hilo lililotokea ndani ya eneo la 18 la Simba lilisababisha mchezo huo kusimama kwa dakika kadhaa na El Shehata kulazimika kupata huduma ya kwanza huku akionekana kuumia zaidi karibu na sehemu ya jicho la kulia.
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha katika juhudi za kusaka matokeo aliwatoa Kapombe na Kanoute na kuwaingiza Israel Mwenda na Miquisonne, baadaye akamtoa Kibu na nafasi yake kuingia Willy Onana.
Pia Benchikha aliwatoa Saido Ntibazonkiza ambaye nafasi yake aliingia Jobe Omar na Clatous Chama ambaye nafasi yake aliingia Freddy Koublan.
Hii ni mara ya nne Simba kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa miaka ya karibuni na sasa timu hiyo kama ilivyo kwa hasimu wake Yanga, wote wanarudi nyumbani kwenye Ligi Kuu NBC na Kombe la FA kusaka tiketi ya kushiriki ligi hiyo kubwa barani Afrika kwa msimu ujao.
Kimataifa Simba nayo yatolewa Ligi ya Mabingwa
Simba nayo yatolewa Ligi ya Mabingwa
Read also
