Madrid, Hispania
Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Hispania, (RFEF) Luis Rubiales amehoji hatua ya kumshitaki mahakamani kwa kumpiga busu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso kwamba imekuja kwa sababu yeye ni mwanaume.
Rubiales anajiandaa kupanda mahakamani kwa kosa la kumbusu mdomoni mshambuliaji huyo wa Hispania wakati wa hafla ya utoaji tuzo baada ya Hispaia kuibwaga England, Agosti mwaka jana na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake mjini Sydney, Australia.
Tukio hilo ambalo limeibua mjadala duniani kote lilisababisha Rubiales kujiuzulu nafasi yake ya urais wa RFEF baada ya kushinikizwa kufanya hivyo huku Jenni na wachezaji wenzake wakidai kwamba tukio hilo limewashushia heshima na halikufanyika kwa makubaliano.
Akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini Hispania, Rubiales alikana kufanya kosa lolote na kuongeza kwamba haiwezekani kuumuliza Jenni kuhusu suala hilo badala yake anaulizwa yeye kwa sababu ni mwanaume.
“Mnaweza kuniuliza mimi hilo kwa sababu mimi ni mwanaume,, kwangu mimi hakuna kosa lolote dhidi ya Jenni, kwa yeyote aliyeona picha za tukio lile, siwezi kuelewa iwapo kuna mtu ataliona tukio lile kuwa ni la udhalilishaji kijinsia,” alisema Rubiales.
Rubiales apia alisema kuwa wahanga wa tukio hilo ambalo liligeuka mjadala katika nchi nyingi hasa za Ulaya ni familia yake pamoja na marafiki zake.
Waendesha mashitaka nchini Hispania wanataka Rubiales afungwa miaka miwili na nusu jela kwa makosa mawili anayotuhumiwa ya ubabe akidaiwa alimlazimisha Jenni kumpiga busu pamoja na udhalilishaji kijinsia.
Rubiales ambaye alikuwa beki enzi zake za soka la ushindani, alisema kwamba labda alitakiwa kuwa kimya bila kufurahia baada ya Hispania kushinda bao 1-0 dhidi ya Engla na kubeba Kombe la Dunia.

Ukiachana na sakala hilo, Rubiales pia alikamatwa juzi Jumatano akihusishwa na tuhuma za kupokea rushwa akidaiwa kupewa mgao usio rasmi wakati wa majadiliano ya kuandaa mechi ya Spanish Super Cup nchini Saudi Arabia.
Akizungumzia tuhuma hizo, Rubiales ambaye akaunti zake zimefungiwa alisema kwamba hajawahi kuchukua rushwa katika maisha yake na kuzitaja tuhuma anazohusishwa nazo kuwa ni uwongo.
“Wamefungi akaunti zangu, na kwa sasa siwezi hata kulipia kinywaji, kama kuna uchunguzi unaofanywa basi hapo kuna hisia kwamba sina kosa,” alisema Rubiales.