London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kwamba Manchester City ipo katika kiwango bora ambacho hakijawahi kuonekana hapo kabla ingawa alidai kuwa Arsenal nao wanaelekea katika ubora huo huo.
Arteta ametoa kauli hiyo wakati kesho Jumapili timu yake itakuwa wageni wa Man City kwenye dimba la Etihad, mechi ambayo itachezwa wakati Arsenal ikishika usukani wa Ligi Kuu England (EPL) kwa tofauti ya pointi moja mbele ya City.
Man City inashika nafasi ya tatu katika EPL, Liverpool ikiwa ya pili wakati timu zote kila moja ikiwa imecheza mechi 28 za ligi hiyo.
“Ni mechi kubwa kwa timu zote, itatupa nguvu kubwa kama tukishinda ingawa bado kuna mechi nyingine nyingi za kucheza baada ya hiyo,” alisema Arteta.
Man City itaingia uwanjani ikipambana kusaka taji la nne mfululizo la EPL ikiwa imeshinda mechi 12 kati ya 13 za ligi dhidi ya Arsenal ambapo mechi pekee iliyopoteza ni kipigo cha bao 1-0 kwenye dimba la Emirates mwanzoni mwa msimu huu.
Kwa Man City pia ushindi wa leo utakuwa na maana kubwa kwani itakuwa mwanzo wa mafanikio yao katika kampeni ya kusaka mataji matatu kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.
Mbali na EPL, Man City pia ipo katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikijiandaa kukabiliana na Real Madrid lakini pia ipo katika nusu fainali ya Kombe la FA ikisubiri kuumana na Chelsea.
“Man City wamepanda kiwango cha juu ambacho hakijawahi kuonekana hapo kabla kwenye soka, tuna wajibu wa kuendana na kasi hiyo na hicho ndicho tunachojaribu kukifanya,” alisema Arteta.
Arteta aliongeza kuwa Man City imepata haki ya kuangaliwa na kila mtu kama mfano wa kuigwa lakini pia imesaidia kwa Arsenal kukuza ubora wake na mahitaji na kujaribu kuwa kama wao na kutaka kuwashinda.
