Na mwandishi wetu
Simba leo Ijumaa imeanza vibaya mbio za kuisaka tiketi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya kwanza ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Bao hilo pekee lililoibeba Ahly lilipatikana dakika ya tano ya mchezo huo mfungaji akiwa ni Ahmed Koka ambaye aliyatumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Simba kujichanganya na kuupiga mpira uliomshinda kipa Ayoub Lakred.
Inonga aliokoa vibaya mpira uliotokea upande wa kushoto wa Simba na kuelekea lango la Simba na Lakred kuokoa hivyo kufuta kosa hilo lakini Koka aliuwahi mpira huo na kuujaza wavuni.
Simba licha ya kufungwa bao hilo lakini walionesha uhai kwa muda wote wa dakika 90 kwa kuuanza mchezo kwa kasi na kutoa dalili zote za kutoka na ushindi.
Dakika ya kwanza tu ya mchezo huo Simba walitengeneza shambulizi lililozaa kona iliyochongwa na Clatous Chota Chama na kuunganishwa kwa kichwa na Kanoute lakini mpira huo ulipaa juu ya lango la Ahly.
Juhudi za Simba kusaka bao la kusawazisha ziliendelea kwa kulisakama lango la Ahly kwa mashambulizi ya mara kwa mara huku Ahly wakionekana kucheza kwa umakini mkubwa kujihami na kusogelea mara chache mno langoni mwa Simba.
Dakika ya 38, Kibu Denis aliwatoka kwa kasi mabeki wa Ahly na kumuunganishia pasi Kanoute ambaye alifumua shuti kali la chinichini ambalo kipa Mustapha Shabir aliokoa na kuwa kona.
Kona hiyo ilichongwa na Chama na kuzua kizaazaa langoni mwa Ahly kabla ya mpira kumkuta Che Malone ambaye alifumua shuti la juu lililopaa sentimita chache na kutoa nje ya lango.
Kipindi cha pili Simba iliendelea na kasi yake ya kulisakama lango la Ahly ambao waliendelea kuweka nguvu nyingi kwa kujihami wakifanya mashambulizi machache ambayo kuna wakati yaliibua hofu langoni mwa Simba.
Katika juhudi za kusaka bao la kusawazisha, kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alianza kwa kuwatoa Kanoute na baadaye Ntibazonkiza na nafasi zao kuchukuliwa na Willy Onana na Jobe.
Baadaye akawatoa Babacar, Shomari Kapombe na Kibu na nafasi zao kuingia Muzamir Yassin, Israel Mwenda na Luis Miquissone.
Mabadiliko hayo bado hayakuweza kubadili lolote kwani mchezo uliendelea kuwa ule ule wa Simba kufanya mashambulizi mengi na Ahly kujihami huku ikilisogelea mara chache lango la Simba na kufanya mashambulizi yaliyoibua hofu.
Katika mechi hiyo mwamuzi aliwapa kadi za njano Babacar na Inonga wa Simba kwa kucheza rafu wakati kwa Ahly mchezaji pekee aliyepewa kadi hiyo ni Marwan Atia.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inasubiri mechi ya marudiano ugenini jijini Cairo ambapo sasa itahitaji ushindi wa zaidi ya bao moja ili iweze kusonga mbele.
Kimataifa Al Ahly yaipiga Simba 1-0
Al Ahly yaipiga Simba 1-0
Read also