Na mwandishi wetu
Simba SC kesho Ijumaa itaanza mtihani wa kusaka tiketi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri katika mchezo utakaoanza saa 3 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti kwenye ligi zao, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45 katika Ligi Kuu NBC na katika mechi tano zilizopita za ligi imeshinda nne na kufungwa moja.
Ahly ni ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na viporo saba dhidi ya Al Masry iliyopo kileleni wenye pointi 27. Al Ahly ina pointi 14 katika michezo saba waliyocheza ambapo katika michezo mitano iliyopita wameshinda yote.
Simba imefunga mabao 39 na kuruhusu mabao 18 katika mechi zote 19 ilizocheza msimu huu wakati Al Ahly katika mechi saba ilizocheza imefunga mabao 15 na kuruhusu mabao manane kwenye wavu wake.
Kwa takwimu hizo ni wazi timu zote zimeonesha ubora katika kuzitumia nafasi lakini pia safu zao za ulinzi zimeonesha kuruhusu mabao mengi hivyo lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wa kesho.
Mchezo huo utakuwa wa tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu baada ya mara mbili kukutana kwenye michuano mipya ya African Football League (AFL) ambapo walitoka sare katika mechi zote mbili kabla ya Ahly kutinga nusu fainali kwa bao la ugenini.
Simba wanaingia kuikabili Al Ahly bila ya washambuliaji wao wawili waliokuwepo kwenye mechi mbili za AFL; Jean Baleke na Moses Phiri lakini tayari nafasi zao zimezibwa na Pa Omar Jobe na Fredy Michael Koublan.
Kuongezeka kwa kocha Abdelhak Benchikha kumeongeza matumaini kwa Wekundu hao kupata ushindi na kufufua matumaini ya timu hiyo baada ya kuishia hatua ya robo fainali kwa misimu minne iliyopita katika michuano ya Afrika.
Na Benchikha amesema maandalizi yao yamekamilika kwa kiasi kikubwa na anaamini wachezaji wake watapambana na kupata ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wao na Watanzania ambao wanawaunga mkono.
“Maandalizi yetu yamekwenda vizuri, wachezaji wote wapo katika utayari kwa ajili ya mchezo, naamini tutashinda na kitu cha msingi mashabiki waje uwanjani kuishangilia timu yao,” alisema Benchikha.
Kocha Mkuu wa Al Ahly, Marcel Koller amesema: “Tumekuja kamili tukihitaji ushindi, najua mchezo utakuwa mgumu sababu Simba imekuwa ikitusumbua hasa tunapocheza hapa kwao lakini tunajivunia ubora wa timu yetu, tutakuwa makini kuwadhibiti wasitudhuru na kutumia madhaifu yao kuwafunga,” alisema Koller.
