Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Yanga na benchi la ufundi la timu hiyo umemkabidhi kiungo Mudathir Yahya mchezo wao wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema hiyo ni kutokana na mchezaji huyo kujitoa kwake katika kuipambania timu ili kupata matokeo katika mashindano yote inayoshiriki.
“Uongozi na benchi la ufundi kwa pamoja wamekubaliana kuwa mchezo wetu dhidi ya Mamelodi, akabidhiwe kijana kutoka Kizimkazi, Mudathir Yahya, na kaulimbiu yetu kwenye mechi hii ‘Simu ziite tukutane kwa Mkapa’ alisema Kamwe.
Kamwe alisema kuwa staili ya kushangilia ya mchezaji huyo ndiyo iliyosababisha kutoa kaulimbiu hiyo wakiwataka mashabiki zao wapigiane simu ili kwenda uwanjani kuijaza Benjamin Mkapa na kuwapa sapoti ‘wanajeshi’ wao waweze kujituma na kuwapa ushindi.
Kuhusu wachezaji majeruhi kwenye kikosi chao, Kamwe alisema hadi sasa kiungo Zawadi Mauya tayari ameanza mazoezi na yupo tayari kwa mchezo, Kibwana Shomari kwa mujibu wa daktari wa timu Moses Etutu, alisema yupo katika asilimia 60 ya utimamu na bado hajaanza mazoezi.
Na Pacome Zouzoua pamoja na Khalid Aucho wao wapo zaidi ya asilimia 80 ya utimamu wao na wameanza mazoezi lakini kwa upande wa beki, Yao Kouassi bado ni asilimia 50/50 kwani bado hajawa timamu.
Yanga itacheza na Mamelodi Machi 30, mwaka huu kwenye, Uwanja wa Mkapa na timu hizo zitarudiana Aprili 5, mwaka huu nchini Afrika Kusini na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Kimataifa Mudathir ‘akabidhiwa’ rasmi Mamelodi
Mudathir ‘akabidhiwa’ rasmi Mamelodi
Read also
