Rosario, Argentina
Polisi nchini Argentina wanachunguza kuwapo madai ya familia ya mwanasoka maarufu nchini humo, Ángel Di Maria kutishiwa kifo yeye na familia yake katika mji wa Rosario.
Habari hizo zimekuba baada ya kuokotwa kifurushi chenye ujumbe wa kifo ulioelekezwa kwa Di Maria na familia yake kama mchezaji huyo atarudi Argentina na kuchezea moja ya klabu katika mji wa Rosario.
Di Maria, 36 ambaye kwa sasa anaichezea Benfica ya Ureno, hivi karibuni alisema anaweza kurudi nyumbani Argentina na kuichezea klabu yake ya utotoni ya Rosario Central.
“Vitisho vya aina hii vinaleta hali ya wasiwasi katika jamii na hilo ndilo lengo lao, kuwafanya watu waogope, wanachofanya ni kuhusisha watu maarufu katika jamii,” alisema ofisa mmoja wa serikali.
Mji wa Rosario umekuwa ukiandamwa na matukio ya uhalifu kati ya makundi hasimu yanayodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya huku mji huo pia ukitajwa kuwa kama kitovu cha biashara hiyo kwenye nchi nyingine.
Di Maria, nyota wa zamani wa PSG ambaye pia alikuwamo katika kikosi cha Argentina kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 2022, anakuwa mchezaji wa pili kukumbana na tishio hilo, kabla yake nahodha wa Argentina, Lionell Messi naye amewahi kujikuta katika hali kama hiyo.
Katika tukio la Messi, mtu mmoja ambaye hakuweza kufahamika alifyatua risasi katika duka kubwa (supermarket) inayomilikiwa na ndugu wa Messi na baadaye ukakutwa ujumbe uliosomeka, “Messi, tunakusubiri wewe.”
Wiki iliyopita, Serikali ya Argentina ilitangaza nia yake ya kuwasilisha muswada katika baraza la kutunga sheria wenye lengo la kuwaruhusu askari wenye silaha kuingilia kati operesheni ya kupambana na madawa ya kulevya na makosa ya jinai katika mji wa Rosario.
Kimataifa Familia ya Di Maria yatishiwa kifo
Familia ya Di Maria yatishiwa kifo
Read also