Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Willy Onana amesema huu ndio wakati muhimu kwa timu yake kuandika historia mpya Afrika kwa kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Alisema anajua wanaenda kupambana na bingwa mtetezi, Al Ahly hivyo hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini ndio wakati wa kwenda kuonesha ubora wao kwa kutimiza malengo yao ya muda mrefu.
“Binafsi najisikia vizuri kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza, Al Ahly ni kama Real Madrid kwa Afrika, inaweza kuwa kwenye kipindi cha mpito, lakini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wanakuja kivingine.
“Hivyo tunajua tunaenda kucheza na timu kubwa sana barani Afrika, hizi ni nyakati bora kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kuandika historia mpya,” alisema Onana.
Mchezaji huyo alisema kwamba alikuwa akiiangalia Simba ikiishia hatua ya robo fainali, lakini ni wakati wa kwenda kubadili hii historia ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.
“Sijui mipango ya mwalimu (Abdelhak Benchikha) kwenye mchezo huo lakini mimi binafsi niko tayari kwa ajili ya mechi hii kubwa ambayo itatazamwa na watu wengi Afrika,” alisema Onana.
