Rio de Janeiro, Brazil
Mpango wa familia ya mshambuliaji wa Brazil, Neymar Jr kumtoa jela beki wa zamani wa Barcelona, Dani Alves anayekabiliwa na kesi ya kubaka umekwama baada ya familia hiyo kutokuwa tayari kulipa dhamana ya Dola 1.1 milioni.
Taarifa ya baba wa Neymar Jr aitwaye Neymar da Silva Santos Sr ilieleza kuwa awali walimsaidia kwa fedha mchezaji huyo wakati kesi ikiendelea lakini hawatoweza kufanya hivyo tena kwa kuwa mchezaji huyo amekutwa na hatia.
Dola 1.1 milioni zinahitajika kwa ajili ya kumuwekea dhamana beki huyo wa zamani wa Barcelona, AC Milan na PSG ambaye anasubiri rufaa iliyowasilishwa na wakili wake kupinga adhabu ya miaka minne nusu jela aliyopewa kwa kosa la kubaka.
Alves anadaiwa kumbaka msichana mmoja katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona, tukio ambalo inadaiwa alilifanya usiku mmoja wa Desemba 2022 na kukamatwa Januari 2023 ambapo aliwekwa ndani hadi alipohukumiwa na mahakama moja ya mjini Barcelona hivi majuzi.
“Kwa upande wangu, kwa familia yangu hili suala ndio limefika mwisho,” alisema Neymar da Silva Santos Sr katika taarifa ya familia hiyo.
Baba wa Neymar hata hivyo hakuweka wazi ni kiasi gani cha fedha walichompa Alves badala yake alisema kwamba kwa sasa hilo ni suala tofauti kwa kuwa majaji watatu kwa pamoja wametoa hukumu dhidi ya mchezaji huyo.
“Kwa maamuzi ya mahakama ya Hispania ya kumkuta na hatia, kumekuwa na uvumi na shauku ya kulihusisha jina langu na la mwanangu katika jambo hili, kwa sasa jambo hili lipo nje ya uwezo wetu,” alisema Neymar da Silva Santos Sr.
Sambamba na hilo, Neymar da Silva Santos Sr pia alisema kwamba ni matumaini yake kuwa Alves sasa atayapata majibu ya mambo yote yanayomtatiza katika familia yake.
Alves, 40, alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu jela na kwa sasa yuko katika gereza moja lililopo nje kidogo ya mji wa Barcelona akisubiri kutolewa kwa dhamana baada ya wakili wake kuahidi kuikatia rufaa hukumu hiyo.
Katika moja ya hoja zake wakili huyo alikuwa akipinga masharti magumu ya dhamana aliyodai ni kama vile yapo kwa ajili ya watu wenye uwezo kifedha.
Neymar Jr na Alves wamecheza soka pamoja katika klabu za Barcelona na PSG lakini pia waliwahi kuwa pamoja timu ya taifa ya Brazil na kwa sasa Neymar anaichezea A Hilal ya Saudi Arabia.
Rais wa Brazil
Wakati huo huo rais wa Brazil, Luiz Lula da Silva akizungumza katika hafla ya wafanyakazi wake juzi Jumatano pia aliupinga mpango wa Mahakama ya Hispania kumpa dhamana Alves.
“Ni kwa mambo haya ya kukiuka haki sisi hatuwezi kukaa kimya, fedha haiwezi kamwe kununua heshima, fedha ambazo Alves anazo, fedha ambazo kuna mtu amempa haziwezi kulipa jinai ambayo mtu ameitenda dhidi ya mwanamke kwa kumbaka,” alisema Rais Da Silva.
Siku chache baada ya Alves kuhukumiwa, Mahakama Kuu Brazil nayo imepitisha uamuzi wa kumtaka mshambuliaji wa zamani wa timu za Real Madrid, Man City na AC Milan, Robinho kutumikia kifungo cha miaka tisa jela akiwa nchini Brazil kwa kosa la kubaka.
Robinho akiwa na wenzake alikutwa na hatia ya kumbaka msichana mmoja katika baa moja mjini Milan, Italia wakati huo akiwa mchezaji wa AC Milan lakini alihamia Brazil.
Mahakama ya Italia katika hukumu yake ilimkuta mchezaji huyo na hatia na kutaka ahukumiwe akiwa Brazil jambo ambalo limeridhiwa hivi karibuni na Mahakama Kuu Brazil.
Rais Da Silva pia alitetea hatua ya Robinho kuhukumiwa nchini Brazil kwa kosa alililofanya nchini Italia takriban miaka 10 iliyopita akisema mchezaji huyo alihitaji kupewa adhabu kwa kosa hilo.
Alves na Robinho wote wanadaiwa kuwa ni wafuasi wakubwa wa Rais Jair Bolsonaro wa Brazil ambaye alikuwa madarakani kabla ya Da Silva kuchukua nafasi hiyo.
