Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Ihefu FC, Mecky Maxime amesema kusimama kwa Ligi Kuu NBC kunapunguza ari ya upambanaji wa timu yake katika mechi za ligi hiyo.
Nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema wamekuwa na kiwango bora tangu kuanza kwa mzunguko wa pili jambo ambalo limewasaidia kupata matokeo chanya na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo lakini ghafla ligi imesimama.
“Nafahamu ni kalenda ya Fifa lakini hii wakati mwingine huwa inatuharibia, ligi itakapoendelea itatulazimu kucheza mechi tatu hadi nne ili kurudi kwenye kiwango chetu tulichokuwa nacho kabla ya ligi kusimama na si jambo zuri kwa kuwa msimu unaelekea ukingoni na ushindani umeongezeka,” alisema Maxime.
Kocha huyo alisema ili kuepuka hilo atajitahidi wapate mechi nyingi za kirafiki, kitu ambacho si rahisi sana kwa sababu timu nyingi hasa za Ligi ya Championship zipo kwenye mapambano ya kumaliza msimu.
Alisema utaratibu huo unaziumiza timu kubwa ambazo hazina wachezaji kwenye timu za taifa kwani kwa kipindi chote cha wiki mbili ambacho ligi imesimama, timu hizo zinaishia kufanya mazoezi ya wenyewe kwa wenyewe.
