Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ amesema baada ya kutoka nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC malengo yao kwa sasa ni kumaliza katika nafasi tano za juu.
Akizungumza na GreenSports, Baresi alisema uwezo wa kufikia hivyo wanao na hiyo ni kutokana na maboresho waliyofanya kwenye dirisha dogo la usajili.
“Ukweli naridhika na kiwango cha timu yangu hasa kwenye mzunguko huu wa pili, tumekuwa bora sana ndio maana tumeondoka nafasi za chini na sasa tupo sehemu salama.
“Lakini kama kocha na kwa ubora wa timu yangu nitafurahi kama tutamaliza msimu ndani ya tano bora,” alisema Baresi’.
Kocha huyo alisema wamekuwa wakiimarika siku baada ya siku na anachojivunia ni wachezaji wageni kuzoeana mapema na wale waliokuwepo tangu mzunguko wa kwanza msimu huu.
Mashujaa yenye maskani yake Kigoma iliyopanda kushiriki Ligi Kuu NBC msimu huu, kwa sasa ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo ikikusanya pointi 21 katika michezo 21 iliyocheza hadi sasa.
