Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik Ten Hag amemsifia mshambuliaji Amad Diallo (pichani) kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya Liverpool kwenye Kombe la FA na kutaka ushindi huo iwe hatua muhimu ya kuendeleza mafanikio.
Man United Jumapili hii jioni ilitoka na ushindi wa 4-3 dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA na sasa inasubiri kuumana na Coventry katika nusu fainali wakati Chelsea iliyoichapa Leicester 4-2 itaumana na Man City katika nusu fainali nyingine.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120, mabao mengine ya Man United yalifungwa na MacTominay dakika ya 10, Antony dakika ya 87 na Marcus Rashford dakika ya 112 wakati ya Liverpool yalifungwa na Mac Allister dakika ya 44, Salah dakika ya 45 na Elliott dakika ya 105.
“Nimefurahishwa naye (Amad), ni mmoja wa wachezaji ambaye amekumbana na vikwazo vingi, amerudi lakini kuna ushindani mkubwa kwenye namba yake na huwa hapati nafasi ya kucheza kila wakati kama inavyotakiwa,” alisema Ten Hag.
Ten Hag alimpongeza Amad aliyefunga bao hilo dakika ya 120 akiwa ameingia uwanjani dakika ya 85, akisema ameonesha mchango wake kwa kufunga goli lakini anafahamu kwamba ana uwezo huo na anafurahi anaweza kufanya jambo hilo.
Amad, 21, ambaye mwamuzi alimtoa kwa kosa la kushangilia bao hilo kwa kuvua shati, Januari mwaka huu alihusishwa na mipango ya kuuzwa kwa mkopo kutokana na kukosa muda mwingi wa kucheza.
Mchezaji huyo ambaye asili yake ni Ivory Coast hadi sasa amecheza dakika 88 tu katika msimu huu lakini amekuwa na mchango muhimu katika mechi dhidi ya Liverpool akiwa ameingia uwanjani dakika za majeruhi.
Ten Hag ambaye mambo yake ya baadaye Man United yamekuwa mjadala akizungumzia umuhimu wa ushindi huo alisema unaweza kuwa mwanzo wa mafanikio baada ya kupitia kipindi kigumu cha matokeo mabaya.
“Huu unaweza kuwa mwanzo wa mambo makubwa, timu inajiamini na ina nguvu ya kufanya mambo ya kuvutia, unapoifunga Liverpool hapo unakuwa na uwezo wa kumshinda mpinzani yeyote,” alisema Ten Hag.
