Manchester, England
Baada ya Man City kupangwa kucheza na Real Madrid katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha wa City, Pep Guardiola ameibuka na kumfisia kiungo wa Real, Jude Bellingham.
Timu hizo zitaumana Aprili 9 na kurudiana Aprili 17 ambapo Pep amesema Real ya msimu huu imekuwa tofauti ukilinganisha na msimu uliopita na kumpa pongezi Bellingham kwa mchango wake katika hilo.
Msimu uliopita, City waliwatoa Real katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya sare ya bao 1-1 ugenini Bernabeu, City wakiwa nyumbani Ettihad kwenye mechi ya marudiano waliibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Bellingham ambaye alijiunga na Real Julai mwaka jana akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya dola milioni 112, hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 20 katika mashindano yote.
Pep aliombwa ufafanuzi kuhusu ubora wa kiungo huyo ambapo alisema kwamba mchango wa mchezaji huyo umekuwa mkubwa mno kwenye timu.
“Timu (Real Madrid) imekuwa tofauti na ya msimu uliopita, mchango Bellingham upo wazi na tutajaribu kuangalia nini anafanya ili kumdhibiti,” alisema Pep.
Pep pia alikiri kwamba kupambana na Real wakati wote ni changamoto nzito na hakuna wa kubisha hilo kwa kuwa timu hiyo ni ya kipekee na katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wanaweza kutawala kila kitu kutokana na uzoefu walionao wa siku za nyuma.
