Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid,Vinicius Jr ameutaka uongozi wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) kuchukua hatua baada ya mchezaji huyo kukumbana kwa mara nyingine na kadhia ya ubaguzi wa rangi.
Vinicius alikuwa akiizungumzia video ya kwenye mtandao wa X (Twitter) ikimuonesha shabiki wa Atletico Madrid akitoa ishara za ubaguzi wa rangi kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan.
Wakati mchezaji huyo akitoa kauli hiyo tayari mabosi wa Mamlaka ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ wameahidi kulifikisha suala hilo kwenye ofisi ya waendesha mashtaka inayohusika na udhibiti wa makosa ya jinai.
“Nafikiri Uefa mmeshafikiria kuhusu adhabu yao, ni ukweli unaosikitisha kwamba matukio haya yanatokea hata katika mechi ambazo mimi sipo,” alisema Vinicius.
Katika posti yake Vinicius Jr, 23, ameziweka pia akaunti za Uefa na Ligi ya Mabingwa wakati katika taarifa yao La Liga walisema watalifikisha suala hilo kwenye vyombo husika licha ya kwamba mechi husika haikuwa ya La Liga.
Vinicius Jr amejikuta akikumbana na kadhia ya ubaguzi wa rangi mara kadhaa ikiwamo Septemba 2022 katika mechi na mahasimu wao wa Madrid, Atletico ingawa uongozi wa Atletico ulilaani tukio hilo lililofanywa na baadhi ya mashabiki wanaoaminika kuwa wa klabu hiyo.
Juni mwaka jana watu wawili walitozwa faini ya Pauni 51,500 na marufuku ya kuingia kwenye viwanja vya soka kwa miaka miwili baada ya kukutwa na hatia ya kuweka sanamu la kwenye maduka ya nguo lenye ufanano na Robinho karibu na uwanja wa mazoezi wa Real Madrid.
Siku hiyo hyo watu wengine watatu walitozwa faini ya Pauni 4,300 na marufuku ya kuingia kwenye viwanja vya soka kwa mwaka mmoja kwa kosa la kutoa ishara za kushabikia ubaguzi wa rangi katika mechi ya Real Madrid na Valencia.
