Na mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema uwanja utakaojengwa mkoani Arusha utaitwa Dk Samia Suluhu Hassan kama Rais ataridhia hilo.
Ujio wa uwanja huo wa kisasa unaotarajiwa kujengwa hivi karibuni ni kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika za mwaka 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji sambamba na Kenya na Uganda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Jumanne hii, Msigwa alisema uwanja huo utabeba zaidi ya watu 30,000 na unatarajiwa kugharimu mabilioni ya fedha.
“Tunaenda kujenga uwanja mkoani Arusha utaogharimu mabilioni ya fedha, utakaoweza kubeba zaidi ya watu 30,000 na tumepanga Rais Samia akiridhia tutauita Dk Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Kuhusu ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja Benjamin Mkapa, Msigwa alisema Sh bilioni 10 zitatumika kubadilisha viti 60,000 na kuweka vya kisasa vya kukunja ambapo pia kila kiti kitakuwa na namba ili kuwawezesha mashabiki kununua na kupata namba ya kiti atakachokalia.
Katika hatua nyingine, Msigwa alisema kwa sasa kwa kushirikiana na TFF wanataka kuweka nguvu kwa vijana chini ya miaka 20 ili kupata wachezaji watakaocheza fainali za Afrika zitakazofanyika nchini.
“Tunaamini kutakuwa na vijana wenye viwango na uwezo wa kusaidia timu, lakini pia tumefungua milango kwa wachezaji wa nje waje tutawapa hati (pasipoti),” aliongeza.
Soka Uwanja kupewa jina la Rais Samia
Uwanja kupewa jina la Rais Samia
Read also
