Madrid, Hispania
Klabu ya Celta Vigo ya Hispania imemfuta kazi kocha Rafael Benitez baada ya kuwa na timu hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi tisa.
Benitez, 63, kocha wa zamani wa timu za Liverpool, Chelsea na Real Madrid, Juni 20 mwaka jana alijiunga na Celta Vigo na anaondoka akiwa na rekodi ya kushinda mechi tano tu kati ya 28 za La Liga.
Kocha huyo aliyeiwezesha Liverpool kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005, anaiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya 17, ikiwa imejitenga na janga la kushuka daraja kwa tofauti ya pointi mbili.
Kabla ya kujiunga na Celta Vigo, Benitez alikuwa akiinoa Everton inayoshiriki Ligi Kuu England (EPL), timu ambayo pia ilimtimua Januari, 2022.
Mechi ya mwisho ya Benitez akiwa kocha wa Celta Vigo ilikuwa Jumapili iliyopita dhidi ya timu yake ya zamani wa Real Madrid, mechi ambayo alipoteza kwa kipigo cha aibu cha mabao 4-0.
Taarifa ya klabu hiyo kuachana na Benitez ilieleza kuwa pamoja na juhudi za kujitoa kwa asilimia 100 kwa kocha huyo lakini timu haikupata matokeo yaliyotarajiwa na klabu.
“Klabu inapenda kumshukuru kwa dhati Rafa Benitez na wasaidizi wake kwa kujitoa kitaaluma tangu wajiunge na timu hiyo pamoja na juhudi walizokuwa wakizifanya bila ya kuchoka,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Benitez ambaye pia aliiwezesha Chelsea kubeba taji la Europa Ligi mwaka 2013 akiwa kocha wa muda, kwa mara ya kwanza ataishuhudia Celta akiwa nje ya benchi la timu hiyo Jumapili ijayo katika mechi ya La Liga dhidi ya Sevilla.
Mafanikio mengine ya Benitez pia yalionekana katika klabu ya Newcastle aliyoiwezesha kupanda na kucheza EPL kutoka Championship msimu wa 2016-17 lakini pia aliwahi kuzinoa timu za Napoli, Valencia, Inter Milan pamoja na klabu ya Dalian Yifang ya China.
