Na mwandishi wetu
Simba imepangwa kucheza na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati hasimu wake Yanga amepangiwa kucheza na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.
Droo ya mechi za hatua hiyo imefanyika leo Jumanne mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo mechi za kwanza zitachezwa Machi 29 na 30 na marudiano ni kati ya Aprili 5 na 6.
Miamba hiyo ya Tanzania itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa mechi zao za mkondo wa kwanza baada ya timu zote mbili kumaliza nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi.
Droo hiyo pia inaonesha Simba endapo itaiondosha Al Ahly itakutana na mshindi wa mchezo kati ya TP Mazembe ya DR Congo na Petro Atletico ya Angola na Yanga ikiitoa Mamelodi itakutana na mshindi wa mechi kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Matola ajipa matumaini
GreenSports imezungumza na kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola kuzungumzia wanachokiona na mikakati waliyonayo juu ya wapinzani wao ambapo alisema wamepata mpinzani ambaye si mgeni kwao,
Matola alifafanua kuwa wamekutana na Ahly mara nyingi katika miaka ya karibuni hivyo wataandaa njia bora ya kuwakabili ili kutimiza lengo lao.
“Tumeiona droo na tumemjua mpinzani wetu si mwepesi Al Ahly, ni timu bora. Kuelekea mchezo wetu wa kwanza bado tuna wiki mbili na siku kadhaa, tutazitumia siku hizo pamoja na kocha mkuu, Abdelhak Benchikha kuona njia bora za kuwakabili na kuvuka hicho kigingi,” alisema Matola.
Gamondi ajivunia ubora Afrika
Naye kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi (pichani chini) alikiri kuwa wamepangwa na timu bora Afrika yenye wachezaji wenye viwango vya juu na mafanikio makubwa ndani na Afrika kwa ujumla.
Gamondi hata hivyo alisema kwamba hilo haliwezi kuwafanya wahofie kucheza nao sababu wao ni timu namba tano kwa ubora Afrika na wanataka kulithibitisha hilo kwa kuwatoa.
“Katika hatua ya makundi hatukupewa nafasi sababu tulipangwa na timu kubwa za Al Ahly na CR Belouizdad lakini tulipambana na kuonesha uwezo tuliokuwa nao na kumaliza wa pili, tukaenda robo fainali hivyo hata kwenye hatua hii tuliyopo hatutohofia timu, tutacheza mpira wa wachezaji 11 dhidi ya wachezaji 11,” alisema Gamondi raia wa Argentina.

Kwa upande wake mtendaji mkuu wa Yanga, Andrew Mtine alisema: “Huwezi kumchagua mpinzani kwa hiyo tumepokea vizuri matokeo ya droo, kifupi ni kwamba tunaiheshimu Mamelodi kwa mafanikio na ubora walionao lakini tutapambana, sisi ni Yanga na kwa ari tuliyonayo Inshallah tutashinda.”
Kwa upande wa droo ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Future FC itacheza na Zamalek, zote za Misri. Abu Salim ya Libya itacheza na RS Berkane ya Morocco, Rivers United ya Nigeria, imepangwa na mabingwa watetezi USM Algers ya Algeria na Stade de Malien ya Mali itacheza na Drams FC ya Ghana.
