Na mwandishi wetu
Azam FC imeeleza wazi kuwa ipo tayari kumuachia mshambuliaji wake, Prince Dube endapo timu inayomhitaji italipa Dola 300,000 za Marekani ambazo ni zaidi ya Sh milioni 760.
Mshambuliaji huyo juzi aliandika barua ya kuomba kuvunja mkataba wa miamba hiyo ya soka nchini ikiwa imepita miezi sita tangu asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2026.
Ofisa habari wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka za Kazi’ alithibitisha kwa GreenSports kuwa uongoezi umepokea barua ya Dube kuomba kuvunja mkataba na baada ya kujadili wamekubali ombi hilo endapo taratibu za kimkataba zitafuatwa.
“Uongozi umeridhia Dube kuondoka lakini anapaswa kufuata matakwa ya mkataba, kwenye kipengele cha mkataba wake ili kuvunja au kuununua mkataba uliobaki mpaka 2026 anatakiwa kutoa Dola za Marekani 300,000,” alisema Zaka.
Inaelezwa kuwa mshambuliaji huyo hana maelewano mazuri na kocha mkuu, Youssouf Dabo ndio maana anataka kuondoka na alishaanza kuonesha dalili hizo tangu mwanzoni mwa msimu huu akiwa kambini Tunisia.
Haijaweza kueleweka mara moja mchezaji huyo atajiunga na timu gani iwapo ataondoka Azam ingawa tayari klabu kubwa maarufu nchini za Simba na Yanga zimeanza kutajwa.