London, England
Kocha wa Chelsea, Mauricio Pochettino amesema anaungwa mkono na wamiliki wa klabu hiyo licha ya kuibuka presha baada ya kupoteza mechi ya fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Liverpool.
Chelsea Jumapili iliyopita ililala mbele ya Liverpool kwenye mechi ya fainali kwa bao la dakika ya 118 lililofungwa na Virgil van Dijk na kumuwezesha kocha wa Liverpool Jurgen Klopp kubeba taji lake la nane na timu hiyo akiwa tayari ametangaza kujiondoa baada ya msimu huu.
Kitendo cha Chelsea kupoteza mechi mbele ya Liverpool iliyolazimika kuwatumia wachezaji makinda kutokana na janga la majeruhi, kimemuweka Pochettino pagumu na kujikuta akilaumiwa kwa kuongoza timu iliyofanya usajili wa mabilioni lakini haina kitu uwanjani.
Mabilionea wanaomiliki klabu ya Chelsea, Todd Boehly na Clearlake Capital tangu wainunue klabu hiyo Mei 2022 wanadaiwa kutumia Pauni 1 bilioni jambo ambalo ilitarajiwa lingekuwa na faida kwa kuipa ushindi timu hiyo.
“Ndio, ndio, ndio, wananipa sapoti na hata baada ya mechi Todd alinitumia ujumbe mzuri sana,” alisema Pochettino.
“Tunazungumza, niliwasalimia nilipowaona uwanjani na baada ya mechi usiku nilikutana nao na tulizungumza, tulipeana mawazo kuhusu mechi, tulizungumza kuhusu nafasi tulizopoteza ambazo zingetuwezesha kubeba taji kwa sababu nadhani tulicheza vizuri katika dakika 90 na nafikiri timu ilikuwa vizuri,” alisema Pochettino.
Chelsea Jumatano hii usiku itakuwa na mtihani mwingine dhidi ya Leeds United katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA itakayopigwa kwenye dimba la Stamford Bridge huku ikitarajiwa kumkosa nyota wake, Christopher Nkunku ambaye ni majeruhi.
