Manchester, England
Mabao matano aliyofunga Erling Haaland katika ushindi wa 6-2 dhidi ya Luton katika mechi ya Kombe la FA yanadhihirisha kwamba mkali huyo wa mabao wa Man City ameanza upya fujo zake za kutupia kambani.
Kwa ushindi huo wa jana Jumanne, Man City iliyokuwa ugenini imefuzu kucheza robo fainali ya Kombe la FA huku Haaland akiendelea kuweka rekodi mpya na kutoa tahadhari kwa timu pinzani hasa katika Ligi Kuu England (EPL) na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa Haaland hiyo inakuwa hat trick (mabao matatu mechi moja) ya sita kwake tangu atue Man City na anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matano katika mechi moja mara mbili.
Haaland ambaye msimu uliopita alikuwa kinara wa mabao wa EPL, msimu huu umekuwa mgumu kwake kutokana na majanga ya kuwa majeruhi lakini mabao matano aliyofunga jana yanatoa kila dalili za kurudi upya kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.
Man City ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya nne ya mchezo huo, mfungaji akiwa Haaland ambaye aliitumia vizuri pasi ya Kevin de Bruyne.
Dakika 15 baadaye, Haaland aliongeza bao la pili akinufaika tena na ushirikiano wa De Bruyne kabla ya kufunga bao la tatu dakika tano kabla ya mapumziko kwa mara nyingine akitumia pasi ya De Bruyne.
Luton walipambana na kupata bao la kwanza dakika ya 45 lililofungwa na Clarke akiitumia pasi ya Barkley kabla ya Clarke kuongeza bao la pili dakika ya 52 akiitumia tena pasi ya Barkley.
Baada ya mabao hayo, Luton walijikuta wakipachikwa mabao matatu mawili yakifungwa na Haaland dakika ya 55 kwa pasi ya De Bruyne na dakika ya 58 kwa pasi ya Bernado Silva wakati bao la sita la Man City lilifungwa dakika ya 72 na Kovacic kwa pasi ya Stones.
Kimataifa Haaland aanza fujo za mabao
Haaland aanza fujo za mabao
Read also
