Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Fred Minziro amesema ushindi wa mabao 2-1 walioupata jana Jumapili dhidi ya Ihefu umetokana na wachezaji wake kufuata kikamilifu kile alichowaelekeza mazoezini.
Minziro aliyewahi kuinoa Yanga, alisema walilazimika kubadili mfumo walioanza nao baada ya wapinzani wao Ihefu kuziba njia zote walizopanga kuzitumia na hiyo iliwasaidia kupata bao la ushindi.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata kile nilichowaelekeza na kupata ushindi, ulikuwa mchezo mgumu uliohitaji mbinu ili kupata ushindi na ndivyo tulivyofanya, malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri mechi zijazo,” alisema.
Naye kocha mkuu wa Ihefu, Mecky Maxime aliwapongeza wapinzani wao kwa ushindi huo lakini akaeleza kuvutiwa na ushindani ambao umeoneshwa na timu yake pia.
“Hongera kwa Kagera sababu wamepata pointi zote tatu lakini niseme mchezo ulikuwa ’50-50′ yoyote angeweza kushinda, pamoja na kupoteza mchezo huu lakini vijana wangu walicheza vizuri na kutoa upinzani mkubwa, tunakubali matokeo na sasa tunaangalia mechi zijazo,” alisema Maxime.
Kwa matokeo ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera imepanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC na kufikisha pointi 21.
Kipigo hicho kwa Ihefu kimeiacha katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi zao 19 walizovuna kwenye michezo 17 waliyocheza hadi sasa.
