Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Saidi amesema mikakati yao kuelekea mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kuongeza hamasa kwa wachezaji na benchi lao la ufundi kuzidi kufanya vizuri kwenye hatua hiyo.
Yanga juzi Jumamosi ilikata tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.
“Lengo letu ni kuwaongezea ari ya upambanaji wachezaji wetu. Awali lengo letu lilikuwa kufika makundi na wamefanya hivyo, na katika hatua hii, baada ya kuwajua wapinzani wetu tukasema tucheze na tutakubali matokeo yoyote, nafurahi kuona tumetinga robo fainali.
“Sasa baada ya kufika robo fainali, lengo letu ni kuongeza hamasa kwa wachezaji wetu na benchi la ufundi ili tushinde na hilo likitokea tutaongeza bonasi nyingine zaidi ya ilivyokuwa hatua zilizopita na ikishindikana hatuwezi kuwadai sababu hapa tulipofika tumevuka malengo tuliyokuwa tumejiwekea,” alisema.
Wakati Hersi akizungumza hayo, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi alisema kiu yake ni kuiona Yanga inafika mbali zaidi ya hapo na anaamini hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chake lakini pia ugumu waliokutana nao kwenye mechi za makundi.
“Tuna kikosi bora sana ambacho kama tukiongeza umakini tunaweza kufanya makubwa zaidi ya haya ingawa baadhi ya watu walitubeza baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Belouizdad kwao, najivunia sana ubora wa wachezaji wangu na sapoti ya mashabiki, miaka 25 kukaa bila kufika hapa si jambo dogo,” alisema Gamondi.
Yanga ambayo msimu uliopita ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika imevuna kitita cha Dola za Marekani 900,000 ambazo ni sawa na Sh bilioni 2.4 baada ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Soka Hersi aweka mikakati ya robo fainali Afrika
Hersi aweka mikakati ya robo fainali Afrika
Read also
