Na mwandishi wetu
Simba imetoka sare ya 0-0 na Asec Mimosas katika mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika, matokeo yanayoifanya Simba ilazimike kushinda mechi ijayo na Jwaneng Galaxy ili kufuzu hatua ya mtoano.
Matokeo ya mechi hiyo iliyopigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Houphouet-Boigny mjini Abidjan, yanazifanya timu tatu zilizobaki katika kundi hilo za Simba, Jwaneng na Waydad kila moja kuwa na nafasi ya kusonga mbele kuungana na Asec ambayo tayari imefuzu.
Asec ndiyo inayoshika usukani katika kundi hilo ikiwa na pointi 11 ikifuatiwa na Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita wakati Jwaneng ni ya tatu ikiwa na pointi nne na Wydad inaburuza mkia na pointi tatu.
Jwaneng na Wydad zitaumana Jumamosi hii, mechi ambayo Jwaneng itakuwa nyumbani na kama ikishinda itafikisha pointi saba.
Kwa mantiki hiyo mechi ya Simba na Jwaneng itakayopigwa Machi 2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ndiyo itakayoamua nafasi ya Simba kusonga mbele au kuziaga fainali hizo, Simba itatakiwa kushinda.
Jwaneng licha ya kuwa nyuma ya Simba kwa pointi lakini si timu ya kubeza hata kidogo, ushindi wa mechi yake na Wydad au sare vyote vitaiweka Simba pagumu na kuwa na ulazima wa kushinda mechi ya Machi 2.
Hata kama Jwaneng itafungwa na Wydad, bado Simba itahitaji kuwa na ulazima wa kupambana ili kupata ushindi katika mechi na Jwaneng kwani kucheza mechi kwa lengo la kutafuta sare pia ni jambo gumu.
Jwaneng akifungwa na Wydad halafu akaifunga Simba, Jwaneng atasonga mbele kwa kuizidi Simba kwa pointi moja.
Kimataifa Simba, Asec hakuna mbabe
Simba, Asec hakuna mbabe
Read also