Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo ameshangazwa na ushindani mkubwa wa Ligi Kuu NBC na kukiri ni ligi bora huku akiwataka wachezaji wake kuongeza bidii ili kuendana na ushindani uliopo kwenye mbio za kuwania ubingwa.
Dabo, raia wa Senegal alieleza kuwa kwa namna ushindani ulivyo hivi sasa kila mchezaji anatakiwa kujitoa kwa asilimia 100 ili kupata uhakika wa pointi tatu katika kila mchezo wa ligi wanaocheza.
“Kwa namna ushindani ulivyo ni kweli Ligi ya Tanzania ni miongoni mwa ligi bora Afrika ndio maana nimewataka wachezaji wangu kuongeza bidii ikiwemo kujitoa kupigania pointi tatu katika kila mchezo wa ligi,” alisema Dabo.
Alisema anafurahishwa na mapambano ya vijana wake lakini amewataka kuongeza zaidi kama ilivyo kwa wapinzani wao Yanga na Simba ili kufikia malengo ambayo wamekusudia kuyafikia mwishoni mwa msimu huu.
Kocha huyo alisema anajivunia ubora wa kikosi chake ambacho kinaundwa na wachezaji wengi wenye vipaji na uzoefu wa mashindano makubwa hivyo amewataka kutumia kila walichokuwa nacho ili kuhakikisha Azam FC inabeba taji la ligi kuu msimu huu.
Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 36 sawa na Simba iliyopo nafasi ya tatu lakini Azam ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na ipo mbele kwa mchezo mmoja.
Soka Ushindani ligi kuu wamshangaza Dabo
Ushindani ligi kuu wamshangaza Dabo
Read also
