Munich, Ujerumani
Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel atalazimika kuachana na timu hiyo Juni mwaka huu baada ya msimu huu wa 2023-24 kumalizika licha ya kuwa mkataba alionao unafikia mwisho Juni 2025.
Tuchel alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Bayern mwezi Machi mwaka jana akichukua nafasi ya Julian Nagelsmann lakini amejikuta akilazimika kusitishiwa mkataba kutokana na mipango mipya ya klabu hiyo.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea aliiwezesha Bayern kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ msimu uliopita lakini kwa sasa anapitia kipindi kigumu hali ambayo imemfanya alazimike kuondoka. Kwa sasa Bayern imeachwa na vinara wa Bundesliga Bayer Leverkusen kwa tofauti ya pointi nane, hiyo ni baada ya kupokea vipigo mfululizo katika mechi za hivi karibuni.
Miongoni mwa vipigo hivyo ni kile cha mabao 3-0 mbele ya Leverkusen na tayari wamepoteza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoano kwa kichapo cha bao 1-0 mbele ya Lazio.
Akizungumzia mpango wa kusitishwa kwa mkataba wa Tuchel, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Jan-Christian Dreesen alisema pande mbili zimekubaliana kusitisha mkataba baada ya mazungumzo ambayo alisema yalikuwa ya wazi.
“Lengo letu ni kufanya maboresho katika michezo kwa kuwa na kocha mpya katika msimu wa 2024-25 tofauti na hilo kwa sasa kila mmoja katika klabu anapambana na changamoto ya kusaka mafanikio makubwa kadri iwezekanavyo kwenye Ligi ya Mabingwa na Bundesliga,” alisema Dreesen.
Tuchel ambaye pia amewahi kuzinoa timu za PSG na Borussia Dortmund alisema ataondoka baada ya msimu huu lakini kwa sasa yeye na makocha wenzake wanafanya kila wawezalo kuhakikisha timu inapata mafanikio makubwa.