Berlin, Ujerumani
Ujerumani ndiye mwenyeji wa fainali za soka za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024, nchi hiyo imeamua fainali hizo hazitoishia kwenye soka tu, bali suala la utunzaji mazingira nalo limepewa kipaumbele.
Habari ya hivi karibuni ya DW imeeleza kuwa wanamazingira nchini humo wamepongeza mpango huo unaosimamiwa na Shirikisho la Soka Ujerumani (DFD) kwa kushirikiana na Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) ingawa wamesisitiza mkazo zaidi katika suala hilo.
Katika kulifanyia kazi jambo hilo wenyeji wametoa vipeperushi vyenye kauli mbiu ya Msimamo Mmoja wa Mazingira Endelevu katika Uefa Euro 2024, michuano itakayoanza Juni 14 na kufikia ukomo Julai 14, 2024.
Moja ya hatua zinazofanyiwa kazi na wenyeji wa Euro 2024 ni kuweka mazingira ya kuzuia ongezeko la hewa ukaa ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.
Katika hilo wenyeji wanaanda mpango wa usafiri wa umma kwenye miji yote ambayo ina viwanja vitakavyotumika kwa fainali hizo huku magari ya umeme na baiskeli pia vikitajwa kuwa ni aina ya usafiri unaotumiwa nchini Ujerumani na utasaidia katika hilo.

Zaidi ya hilo viwanja vyote 10 ambavyo vitatumika kwa mechi za fainali za Euro 2024, umeme wake utakuwa ni ule wa nishati jadidifu (renewable energy) nishati ambayo imekuwa ikihimizwa na wanamazingira dunaini kote kwa kuwa ni nishati salama kwa mazingira.
Mpango mwingine wa wenyeji katika utunzaji mazingira ni kudhibiti takataka za vyakula na nyinginezo kutokana na ugeni ambao utakuwa nchini Ujerumani kwa kipindi chote cha fainali hizo.
Katika hilo mpango uliopo ni kuwa na matumizi ya vifaa sahihi vya kubebea chakula vinavyoweza kutumika zaidi ya mara moja badala ya vile vinavyotumika mara moja na kutupwa.
Akiupongeza mpango huo, mkuu wa idara ya huduma ya Mazingira, Thomas Fischer alisema anaamini Ujerumani ambayo aliitaja kuwa ni nchi ya soka ina fursa nzuri za kuandaa fainali za Euro za kipekee na za mfano kwa wakati wote zitakazojali utunzaji mazingira.
Fischer pia alisema kwamba wanamazingira wangependa kuona viwanja vinakuwa na sehemu kubwa ya maegesho ya baiskeli na kuzuia magari viwanjani huku akitaka timu ya taifa ya Ujerumani iwe mfano kwa kuachana na usafiri wa ndege badala yake watumie treni.