Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola pamoja na kukiri kwamba mchezo wao wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas utakuwa mgumu lakini hawapo tayari kupoteza mchezo huo.
Simba tayari ipo Ivory Coast kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Le Felicia, Abidjan kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na miamba hiyo ya Tanzania inalazimika kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali.
Akizungumza na mtandao wa timu hiyo Matola alisema wanatambua ubora wa wapinzani wao, ni timu yenye wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa na haijapoteza mchezo katika hatua hiyo ya makundi lakini kutokana na uhitaji wa matokeo wamewaandaa wachezaji wao kupambana ili kurudi na ushindi.
“Tunajua wenzetu wapo nyumbani na ni timu ambayo imekamilika na ndio vinara kwenye kundi letu lakini hata Simba si timu dhaifu, kabla ya kuja huku tumefanya maandalizi mazuri yenye lengo la kutupa ushindi lakini hata wachezaji tuliokuja nao wanajua umuhimu wa ushindi kwa hiyo tupo tayari,” alisema Matola.
Matola alisema kurejea kikosini kwa beki Henock Inonga kumeongeza matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo kutokana na uzoefu aliouonesha kwenye michuano ya Afcon.
Akizungumzia kuhusu kukosekana kwa kipa wao, Ayoub Lakred, Matola alisema kwamba hilo ni pigo lakini uwepo wa Aishi Manula na Ally Salim unawafanya waamini kuwa wapo sehemu salama.
Asec inaongoza Kundi B kwa pointi 10, Simba inashika nafasi ya pili pointi tano, Jwaneng Galaxy ya tatu kwa pointi nne na Wydad AC inaburuza mkia kwa pointi tatu.
