Munich, Ujerumani
Mambo si mambo katika klabu ya Bayern Munich ambayo imeendelea kuyumba katika Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga kwa kupoteza mchezo wa tatu mfululizo katika siku zisizozidi tisa.
Kipigo cha jana Jumapili cha mabao 3-2 mbele ya VfL Bochum ni mwendelezo wa matokeo yasiyo ya kuridhisha kwa timu hiyo kongwe na yenye historia ya kuvutia licha ya kocha Thomas Tuchel kudai kwamba wana uwezo wa kubadili mambo.
Katika mechi na Bochum, nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, Harry Kane ambaye nyota yake ya mabao imeendelea kuonekana katika timu hiyo, alifunga bao lakini hakuweza kuiokoa timu yake na janga la kupoteza pointi tatu.
Bayern walikuwa kwanza kupata bao lililofungwa na Jamal Musiala dakika ya 14 lakini Bochum walijibu mapigo kwa kufunga mabao mawili ya Takuma Asano na Keven Schlotterbeck katika dakika za 38 na 44.
Bochum waliongeza bao la tatu dakika ya 78 lililofungwa na Kevin Stoger kwa penalti na dakika ya 87 Kane alifunga bao la pili kwa Bayern ambalo ni bao la 25 kwake, bao ambalo liliongeza idadi ya mabao aliyofunga lakini majanga ya Bayern yaliendelea kuwa vile vile.
Mara ya mwisho Bayern kupoteza mechi tatu mfululizo ilikuwa Mei 2015 wakati timu hiyo ikinolewa na kocha wa sasa wa Man City, Pep Guardiola na sasa chini ya Thomas Tuchel (pichani juu) hali hiyo imejirudia katika namna mbaya.
Mwenendo wa timu katika mechi na Bochum haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo, walikosa uvumilivu na kuanza kurusha mipira ya tenisi uwanjani na wakati mwingine kumlazimisha mwamuzi asimamishe mchezo.
Bayern wamekuwa vinara wa Bundesliga kwa misimu 11 iliyopita lakini msimu huu wanaonekana kuwa na mtihani mgumu kufanikisha jambo hilo na kibaya zaidi huenda wakamaliza msimu bila taji.
Timu hiyo tayari imeharibu kwenye German Super Cup kama ilivyo kwenye German Cup na hali pia si nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, tayari imelala kwa bao 1-0 mbele ya Lazio katika mechi yake ya kwanza ya hatua ya 16 bora.
Tuchel, kocha wa zamani wa Chelsea anauona ugumu wa kubeba taji la Bundesliga msimu huu lakini hapo hapo anadai kuwa wakijiamini wanaweza kufanya kweli kama ilivyokuwa msimu uliopita juhudi zao zilivyowalipa kwa hiyo na msimu huu wataendelea kupambana.
Katika Bundesliga Bayern inashika nafasi ya pili ikiwa imeachwa kwa tofauti ya pointi nane na vinara wa ligi hiyo, Bayer Leverkusen lakini pia inafukuziwa na Stuttgart inayoshika nafasi ya tatu ikiwa imetanguliwa na Bayern kwa tofauti ya pointi nne, timu zote hizo zimecheza mechi 22.
Matokeo ya mechi za Bundesliga jana Jumapili
VfL Bochum 3-2 Bayern Munich
Freiburg 3-3 Frankfurt
Kimataifa Mambo si mambo Bayern Munich
Mambo si mambo Bayern Munich
Read also
