Lausanne, Switzerland
Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imekataa kubadili kanuni zake ili kumruhusu bondia mkongwe, Manny Pacquiao ashiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris baadaye mwaka huu licha ya kuwa na umri wa miaka 45.
IOC imeiandikia barua Kamati ya Olimpiki ya Philippine ikieleza kuwa haiwezi kubadili kanuni zake ili kumruhusu Pacquiao ashiriki katika mchezo wa ngumi na miaka 45 wakati umri uliopo katika kanuni za IOC ni miaka 40.
Pacquiao ambaye alistaafu kucheza ngumi mwaka 2021, anataka kushiriki katika ngumi kwenye Michezo ya Olimpiki jijini Paris akiwa na miaka 45 jambo ambalo limekataliwa na IOC.
Katika taarifa ya IOC iliyopatikana jana Jumapili, maofisa wa olimpiki nchini Philippine anakotokea bondia huyo wameelezwa kuwa umri uliowekwa wa bondia kutozidi miaka 40 utabaki hivyo hivyo.
Mwaka 2013, umri wa mabondia kushiriki Michezo ya Olimpiki uliongezwa kutoka miaka 34 hadi 40, uamuzi ambao ungemuwezesha Pacquiao kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016 lakini alikataa, kipindi ambacho pia alichaguliwa kuwa seneta nchini Philippine.
Pacquiao ni mmoja wa mabondia maarufu duniani, alistaafu ngumi akiwa na miaka 42 na kuacha rekodi ya kucheza mapambano 72 na kushinda mikanda 12 yenye hadhi ya kimataifa katika uzito tofauti tofauti.
Ngumi IOC yamzuia Pacquiao kushiriki Olimpiki
IOC yamzuia Pacquiao kushiriki Olimpiki
Read also
