Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe inadaiwa amewaarifu mabosi wa klabu yake ya PSG ya Ufaransa kuwa ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Mbappe, 25, mkataba wake na PSG unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu na kwa muda sasa amekuwa akihusishwa mno na mipango ya kujiunga na klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Uamuzi wa Mbappe umekuja ikikumbukwa msimu uliopita aliingia kwenye mgogoro na mabosi wa PSG waliomtaka aongeze mkataba au auzwe lakini baadaye utata huo ulimalizwa na pande zote mbili.
Chanzo cha mgogoo huo ni msimamo wa mabosi PSG kutokuwa tayari kuendelea kubaki na mchezaji huyo kwa hofu kwamba angeondoka bila ya wao kupata chochote na kumtaka asaini mkataba mpya jambo ambalo Mbappe hakuliafiki.
Wakati mgogoro huo ukiendelea, Mbappe aliadhibiwa kwa kuachwa kwenye kikosi cha kwanza cha PSG kilichokuwa katika ziara za Asia kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu wa 2023-24.
Katika makubaliano hayo inadaiwa kuwa ingawa Mbappe hakuongeza mkataba kama walivyotaka mabosi wa PSG lakini inadaiwa kwamba katika makubaliano yao, klabu hiyo itafaidika mchezaji huyo akiuzwa.
Hatua ya Mbappe kueleza dhamira yake ya kuondoka baada ya msimu huu, imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kigogo mmoja wa PSG kudai kwamba anataka mchezaji huyo abaki PSG.
Mwishoni mwa msimu wa 2021-22, Mbappe alitajwa kuwa angeondoka kagtika klabu hiyo lakini alikubali kusaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao unaishia mwishoni mwa msimu huu.
Kuondoka kwa Mbappe kutaifanya PSG iwe imeachana na majina makubwa matatu yaliyotamba katika misimu mitatu iliyopita baada ya Neymar na Lionel Messi kuondoka msimu uliopita.
Kimataifa Mbappe atangaza kuondoka PSG
Mbappe atangaza kuondoka PSG
Read also
