Na mwandishi wetu
Msafara wa Yanga uliojumuisha wachezaji 25 na viongozi 11 wa benchi la ufundi upo Morogoro kwa ajili ya mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu NBC dhidi ya KMC utakaochezwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Yanga iliyomaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 40 katika michezo 15, imedhamiria kushinda mchezo huo dhidi ya KMC ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao kwa msimu wa tatu mfululizo.
“Ni mchezo mgumu sana, KMC ni kati ya timu zilizofanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza ndio maana ipo nafasi ya nne, kwa kulijua hilo ndio maana tumekuja na wachezaji wetu wote kuhakikisha ushindi unapatikana,” alisema meneja wa Yanga, Walter Harrison.
Meneja huyo alisema mbali na kutaka ushindi lakini wamepanga kuutumia mchezo huo kama maandalizi ya kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad.
Alisema wachezaji wao wote wakiwemo Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na Mahtlas Makudubela ‘Skudu’ wapo fiti na wamejumuishwa kwenye msafara huo na kazi inabaki kwa benchi lao la ufundi kama watahitaji kuwatumia au kuendelea kuwapumzisha.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, timu hiyo ya Jangwani iliibugiza KMC mabao 5-0.
Soka Yanga yaifuata KMC Morogoro
Yanga yaifuata KMC Morogoro
Read also
