Nairobi, Kenya
Mwanariadha wa Kenya, anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za Marathon, Kelvin Kiptum (pichani) amefariki dunia na kocha wake katika ajali ya gari iliyotokea jana Jumapili jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Kiptum aliyekuwa akipewa nafasi kubwa kutamba kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris baadaye mwaka huu, amefariki baada ya gari alilokuwa akiendesha kuacha njia na kugonga mti.
Kutokana na umri wake, mdogo wa miaka 24, Kiptum alikuwa akitajwa kuwa mmoja wa wanariadha ambao walipewa nafasi kubwa ya kubeba medali katika mashindano mbalimbali makubwa duniani.
Kifo cha mwanariadha huyo pia kimemgusa Rais William Ruto wa Kenya ambaye katika taarifa yake mbali na kutuma salamu za rambirambi pia amemtaja mwanariadha huyo kuwa ni mtu wao wa baadaye akimaanisha alivyokuwa na sifa za kutamba kwenye riadha.
Kiptum akiwa na kocha wake, Gervais Hakizimana raia wa Rwanda, kwa mujibu wa polisi walipata ajali hiyo saa tano usiku karibu kabisa na mji wa Kapsabet nchini Kenya.
Mtu mwingine aliyekuwa kwenye gari hilo ni msichana wa miaka 24 ambaye kwa mujibu wa polisi aliwahishwa hospitali akiwa amejeruhiwa vibaya wakati Kiptum na Hikizimana walifariki hapo hapo.
Wanariadha na wanafamilia ya Kiptum akiwamo baba yake walifika katika chumba cha kuhifadhia maiti baada ya taarifa za vifo hivyo kusambaa kwenye vyanzo mbalimbali vya habari.
Kiptum ni mwanariadha wa kwanza kuweka rekodi ya kukimbia na kumaliza mbio za marathon kwa muda usiozidi saa mbili, rekodi aliyoiweka Oktoba mwaka jana katika Chicago Marathon na hivyo kuvunja rekodi ya Mkenya mwenzake, Eliud Kipchoge.
Katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, Kiptum na Kipchoge ni kati ya wanariadha waliokuwa wakisubiriwa kwa hamu kuiwakilisha vyema Kenya katika michezo hiyo.
Kiptum anaingia katika orodha ya wanariadha wanne wa Kenya waliofariki dunia kwa ajali ya gari, wengine ni David Lelei aliyefariki mwaka 2010 na Francis Kiplagat na Nicholas Bett ambao walifariki mwaka 2018.
Riadha Mwanariadha Kenya afariki kwa ajali ya gari
Mwanariadha Kenya afariki kwa ajali ya gari
Read also
