Na mwandishi wetu
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amesema anataka kuweka rekodi kwa kuwa miongoni mwa manahodha wa timu hiyo waliobeba ubingwa mara tatu mfululizo.
Akizungumza na GreenSports, nahodha huyo alisema pamoja na kuwa lengo mama la kila mchezaji ni kuipigania timu kufikia malengo iliyopanga mwanzoni mwa msimu lakini akiwa kama nahodha taji la tatu litakuwa na maana kubwa kwake.
“Nataka kuwemo kwenye rekodi ya kuwa nahodha niliyebeba mataji matatu mfululizo nikiwa na Yanga na hayo ndio malengo ya kila mmoja wetu kuipigania timu kutimiza kile tulichokikusudia ambacho ni kutetea mataji yote,” alisema Mwamnyeto.
Alisema kwa namna walivyojipanga, anaamini hilo litatimia kwani wana kikosi imara chenye wachezaji wenye uchu wa mafanikio.
Mbali na Mwamnyeto, manahodha wengine waliobeba mataji zaidi ya matatu waliopita kwenye kikosi cha Yanga ni Fredy Mbuna aliyebeba mataji 13 kwa vipindi tofauti na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyebeba mataji manne ya ligi lakini kwa misimu tofauti.
Yanga imekamilisha mechi za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo wakiwa kileleni mwa msimamo wakikusanya pointi 40 katika michezo 15.
