Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesifu juhudi zilizooneshwa na wachezaji wake katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Ushindi huo umeiwezesha miamba hiyo ya soka nchini kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakikusanya pointi 40.
“Kila mchezaji ametimiza wajibu wake ipasavyo hata washambuliaji wangu walikuwa makini kutumia nafasi kipindi cha kwanza, hii inaonesha namna tunavyozidi kuimarika kuelekea mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema pia amefurahi kuona washambuliaji wake wakiendelea kuimarika kwa kupunguza papara na anaamini hilo litaongezeka zaidi katika mechi zijazo.
Naye kocha mkuu wa Prisons, Hamad Ally alisema mapumziko ya muda mrefu ndiyo yamechangia wapoteze mchezo huo sababu wachezaji wake wamechelewa kuingia kwenye mchezo.
Alisema kipindi cha kwanza walicheza chini sana na kuwaruhusu wapinzani wao kuutawala mchezo na kufunga mabao mawili lakini kipindi cha pili walibadili mfumo ambao anafurahi uliwarudisha mchezoni na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.
“Tungeweza kupata hata pointi moja lakini imekuwa ngumu sababu Yanga ni timu bora ina wachezaji wenye uwezo mkubwa, tunakubali matokeo na tunarudi kujipanga ili kufanya vizuri mechi zijazo,” alisema Hamad.
Soka Gamondi awasifu wachezaji Yanga
Gamondi awasifu wachezaji Yanga
Read also
